CHIMBUKO LA BODI YA MIKOPO YA SERIKALI ZA MITAA
Historia ya Bodi ya Mikopo ya Serikali za Mitaa inaanzia mwaka 1953 wakati wa utawala wa kikoloni ulipoanzisha Taasisi ya Fedha ya Serikali za Mitaa iliyojulikana kama “The Local Council Board” chini ya Sheria ya Serikali za Mitaa (The Local Government Ordinance Cap 333) ya mwaka 1953. Taasisi hiyo kwa wakati huo iliundwa kwa madhumuni ya kuzihudumia Halmashauri za Wilaya na Mamlaka za Wenyeji (Native Authorities); na hata michango iliyokuwa inatolewa kwa ajili ya mtaji wa kuendeshea shughuli za Bodi ilichangwa na Halmashauri za Wilaya na Mamlaka za Wenyeji. Michango hiyo ilitumika kukopesha Mamlaka hizo katika miradi yenye manufaa kwa jamii kama vile Shule, Vituo vya Afya, Ujenzi wa Nyumba za Watumishi, Majengo ya Utawala n.k. Michango pia ilitumika kukopesha Mamlaka za Serikali za Mitaa ili kushughulikia masuala ya Dharura na Majanga.
BODI YA MIKOPO YA SERIKALI ZA MITAA MWAKA 1965 HADI 1972
Kwa kuzingatia umuhimu wa taasisi hii, mwaka 1965 Sehemu ya XII ya Sheria ya Serikali za Mitaa (Cap 333) ya Mwaka 1953 iliyounda “The Local Councils Board” ilifanyiwa marekebisho kwa kupitisha Sheria ya Serikali za Mitaa (Marekebisho) Na. 16 ya mwaka 1965 yaliyowezesha kuundwa kwa Bodi ya Mikopo ya Serikali za Mitaa (The Local Government Loans Board). Mabadiliko hayo yaliziwezesha pia Halmashauri za Miji kuchangia katika Bodi na kupata huduma zilizokuwa zinatolewa na Bodi kama ilivyokuwa kwa Halmashauri za Wilaya. Kabla ya kupitishwa kwa Sheria hiyo ya marekebisho, Halmashauri za Miji zilikuwa zinapata huduma ya mikopo kutoka katika Mfuko wa Mikopo wa Mamlaka za Miji (Urban Local Authorities Loans Fund). Fedha za Mfuko huo zilikuwa zinatolewa na Serikali Kuu kutokana na Bajeti yake ya Maendeleo.
Bodi hii iliendelea kutoa huduma za Mikopo na huduma nyinginezo hadi mwaka 1972 wakati ilipositisha huduma zake baada ya Serikali kuvunja mfumo wa Serikali za Mitaa na kuanzisha mfumo mpya wa utawala uliojulikana kama Madaraka Mikoani. Katika kipindi chote cha kuanzia mwaka 1953 hadi 1972 ambacho Bodi ilikuwa ikitoa huduma, baadhi ya mafanikio yaliyotokana na huduma zake kama ilivyoelezwa hapo awali ni pamoja na ujenzi wa shule, zahanati, majengo ya Utawala/Ofisi, nyumba za kuishi wafanyakazi, zana za kazi (kama magari ya maji safi na taka) n.k
Majengo ya utawala yaliyopo sasa katika Majiji ya Mwanza na Mbeya; Manispaa za Moshi, Dodoma, Morogoro na Bukoba na Halmashauri za Wilaya za Nzega, Rungwe, Mbulu, Arumeru n.k. ni baadhi ya mifano ya mali na huduma zilizotokana na mikopo ya Bodi ya zamani. Hata baadhi ya nyumba za Halmashauri za kuishi watumishi zilizopo sasa zilijengwa kwa mikopo ya Bodi hiyo pia. Aidha, hisa zilizonunuliwa na Halmashauri ya Jiji la Dar-es- Salaam katika Kampuni ya Mwambao Shipping Company zilitokana na fedha za mkopo wa Bodi ya zamani.
Hivyo, Bodi ya Mikopo iliyopo sasa kwa sehemu kubwa imechukua sura ya Bodi ya zamani iliyokuwepo kabla ya kuvunjwa kwa mfumo wa Serikali za Mitaa. Madhumuni yake hayatofautiani sana na yale ya Bodi ya zamani ambayo yanalenga katika kuhakikisha kuwa Mamlaka za Serikali za Mitaa zinakuwa na chanzo kingine cha fedha ambazo zitatolewa kwa njia ya mikopo nafuu, na pia kutoa huduma nyingine kwa faida ya Mamlaka hizo.
BODI YA MIKOPO KIPINDI CHA MWAKA 1972 HADI 1982
Baada ya Serikali kuvunja mfumo wa Serikali za Mitaa na badala yake mfumo wa Madaraka Mikoani kuanza kufanya kazi, Mashirika ya Maendeleo ya Wilaya (District Development Corporations – DDCs) yalianzishwa. Wakati huo huo wazo la kuifanya Bodi kuwa Bodi ya Fedha na Mikopo ya Mashirika ya Maendeleo ya Wilaya liliendelea kufanyiwa kazi. Hivyo, katika hatua za awali za uanzishwaji wa Mashirika ya Maendeleo ya Wilaya jumla ya Sh. 3,901,475/= zilitolewa kama mtaji kwenye mashirika ya maendeleo 35.
BODI YA MIKOPO KUANZIA MWAKA 1982 HADI 1986
Kutokana na uamuzi wa Serikali wa kurejesha mfumo wa Serikali za Mitaa; mwaka 1982 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa Na. 9 ya mwaka 1982, sura ya 290 RE 2002 na 2019, ambayo iliwezesha kuundwa kwa Bodi ya Mikopo ya Serikali za Mitaa ya sasa. Madhumuni ya kuanzishwa kwa Bodi ni kuziongezea Mamlaka za Serikali za Mitaa fursa ya kupata fedha kwa njia ya mkopo ili kutekeleza miradi inayolenga kuchochea shughuli za kiuchumi na kuongeza ajira na mapato ya ndani.
BODI YA MIKOPO KUANZIA MWAKA 1986 HADI 2023
Umuhimu wa kuanzishwa Bodi unatokana na wajibu wa Mamlaka za Serikali za Mitaa katika kujenga na kukarabati miundombinu na kutoa huduma za msingi ili kuchochea shughuli za kiuchumi. Aidha, ugatuaji wa madaraka kwa wananchi umepeleka majukumu zaidi kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa. Vile vile kila Mamlaka inavyo vipaumbele vinavyoendana na mazingira yake ambavyo vinatakiwa vitekelezwe. Utekelezaji wa majukumu hayo unahitaji fedha nyingi ambazo haziwezi kupatikana kutokana na mapato ya kawaida. Kwa maana hiyo, mikopo ya Bodi imekuwa njia ya nyongeza ya kupata fedha kwa madhumuni hayo ili kuziwezesha Mamlaka za Serikali za Mitaa kutimiza malengo yake.
Haki Miliki@ Bodi ya Mikoya Mikopo ya Serikali za Mitaa