Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) imesema itahakikisha inasimamia ipasavyo matumizi ya fedha za umma zilizopelekwa kutekeleza miradi kwenye maeneo mbalimbali na hawatakubali Serikali ipate hasara.
Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) Mhe. Ester Bulaya ameyasema hayo Machi 21, 2024 katika kikao cha majumuisho ya ziara walioifanya Kamati hiyo katika Manispaa ya Moshi, Mkoani Kilimanjaro ya ukaguzi wa jengo la halmashauri, ujenzi wa shule ya sekondari na stendi ya Manispaa ya Moshi.
Ameeleza pamoja na kuonekana kwa ubora wa ujenzi wa miradi katika Mkoa wa Kilimanjaro, Kamati ya LAAC inajukumu la kufuatilia fedha za Serikali ili zifuate utaratibu katika matumizi yaliyopangwa kwa kuzingatia miongozi, taratibu na sheria za Serikali na kutoka Ofisi ya Rais -TAMISEMI.
“Naibu Katibu Mkuu ( Elimu) mtu ambaye amekiuka taratibu lazima ashughulikiwe nchi hii ni kubwa unapopata fursa ya kusimamia fedha za miradi lazima tusimamie ilete tija kwa wananchi,” amesisitiza Mhe. Bulaya
Akisoma maazimio ya Kamati hiyo, Mjumbe wa LAAC, Mhe. Hawa Mchafu(Mb), amesema Kamati imemtaka Mkurugenzi kuhakikisha kasi ya mradi wa jengo la utawala la Halmashauri hiyo inaongezeka na kukamilika ndani ya muda wa mkataba tarehe 28 Machi 2024.
Amesema Kamati imemtaka Mkurugenzi kuhakikisha utekelezaji wa miradi unazingatia sheria, kanuni na taratibu inayotolewa na Serikali ikiwa ni pamoja na kujenga kulingana na michoro illyotolewa na Ofisi ya Rais -TAMISEMI.
Pamoja na maekelezo mengine Kamati pia imeitaka Ofisi ya Rais -TAMISEMI ichukue hatua kwa watu wote waliohusika kwa ukiukwaji wa sheria wakati wa kuingia mkataba wa ujenzi wa stendi.
Naye, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais – TAMISEMI Dkt. Charles Msonde ameahidi Ofisi ya Rais – TAMISEMI itasimamia kwa karibu maelekezo yote ya Kamati iliyoyatoa na yatatekelezwa ikiwamo kuundwa kwa timu ya kufanya tathmini ya ujenzi wa mradi wa stendi ya Manispaa ya Moshi ili hatua zichukuliwe na wananchi wapate huduma.
Haki Miliki@ Bodi ya Mikoya Mikopo ya Serikali za Mitaa