BODI ya Mikopo ya Serikali za Mitaa imesema inakusudia kutoa kipaumbele kwa miradi midogo kwa kuwa miradi hiyo inagusa wananchi moja kwa moja na urejeshaji wake ni wa muda mfupi.
Kwa mujibu wa Katibu wa Bodi hiyo Bwana Richard Mfugale, Bodi yake ilikuwa imejipanga kukopesha halmashauri kiasi cha shilingi bilioni 1.8 lakini kutokana na kukosekana kwa maombi ya fedha kutoka halmashauri hizo, fedha hizo bado hazijaweza kutumika.
Alisema kuwa halmashauri, Majiji pamoja Manispaa nchini zinapaswa kuibua fursa za miradi ya maendeleo na kuziandikia maombi na kisha kuyawasilisha kwa Bodi ya Mikopo ya Serikali za Mitaa kwa ajili ya kuomba mkopo.
Alisisitiza kuwa halmashauri zina wajibu wa kuandaa maandiko ya miradi mbalimbali ya maendeleo na kutuma michanganuo hiyo katika bodi ili iweze kupitiwa na wataalamu wake ili kuona kama imekidhi vigezo vya kupatiwa mikopo husika.
“Kwa sasa ambapo tuna fedha kidogo, tunatakiwa tutoe sapoti miradi midogo yenye tija kwa wananchi, mfano viwanda vidogo vidogo ambavyo mitaji yake haiwezi kuzidi shilingi milioni 50 au 100, hivyo halmashauri zishirikiane na wananchi katika kuibua fursa zilizopo katika maeneo yao,” alisema bwana Mfugale na kuongeza:
“Tunapoenda kuchagiza maendeleo ya watu tunaangalia watu wengi wanajishughulisha na nini, watu wetu wengi wapo kwenye shughuli za kilimo, ufugaji na uvuvi, hivyo katika shughuli hizo hakuhitajiki mabilioni ya fedha, ni fedha kidogo tu lakini zikitumika vizuri zitasaidia kuleta mabadiliko makubwa katika jamii.”
Akitolea mfano wa elimu ya upandikizaji wa samaki mwambao mwa bahari na ziwani amesema utaalamu huo utasaidia kuokoa uharibufu wa mazalia ya samaki pamoja na kuepusha hatari ya kupoteza maisha ya wavuvi pindi wanapofuata samaki katika kina kirefu cha maji.
Alisema faida nyingine ya mikopo kwa makundi hayo itasaidia kununua vifaa vya kisasa vya wavuvi badala ya kutumia makokororo, lakini pia itasaidia kununua mashine za kuchakata mazao yatokanayo na kilimo na ufugaji.
“Tukifanya hivi kwa wavuvi, wakulima na wafugaji tutafanikiwa kuongeza thamani ya bidhaa pamoja na kutoa ajira kwa wananchi, hivyo halmashauri zinatakiwa kushirikiana na wananchi wake ili waweze kuainisha miradi yao pamoja na kuwadhamini, sisi tupo tayari kutoa mkopo,” alisema.
Wakati huo huo bwana Mfugale alisema kuwa Bodi kwa kushirikiana na Benki ya TIB wameanzisha mafunzo ya uandishi wa miradi kwa wachumi, watunza hazina pamoja na maafisa mipango kote nchini kwa lengo la kupata wataalamu wa kuandaa miradi kwani asilimia kubwa walikuwa hawana elimu hiyo.
“Mafunzo haya pia yatazisaidia halmashauri kuandika maandiko ya kitaalamu kwa ajili ya kuombea mikopo kwenye Taasisi za fedha kwani sio lazima wakope kwetu tu, hivyo mbali ya kuviandikia vikundi vyao lakini pia wataomba mikopo yao wenyewe,” alisema.
Alisema malengo ya Bodi ya Mikopo ya Serikali za Mitaa ni pamoja na kuziwezesha Mamlaka za Serikali za Mitaa kuwa na miradi itakayoweza kuinua kipato cha wananchi pamoja na Taifa kwa ujumla hivyo kuzitaka Halmashauri kuitumia Bodi hiyo vizuri kwa kuwa Bodi hiyo imeundwa kwa ajili ya wananchi.
Haki Miliki@ Bodi ya Mikoya Mikopo ya Serikali za Mitaa