Bodi ya Mikopo ya Serikali za Mitaa imesema kuwa inakusudia kuifanyia marekebisho sheria ya serikali za Mitaa Sura ya 290 ili kuipa uhai na kukidhi mahitaji ya sasa pamoja na changamoto zake.
Kauli hiyo imetolewa jana na Katibu wa Bodi ya Serikali za Mitaa bwana Richard Mfugale ofisini kwake mjini Dodoma.
Alisema kuwa Bodi ya wakurugenzi ilikaa na kuipitia sheria iliyopo na kuona kuwa ipo haja ya kuifanyia marekebisho sheria hiyo ili iweze kwenda na wakati.
“Sehemu itakayofanyiwa marekebisho ni Eneo la 5 Sura ya 290 ambapo pamoja na mambo mengine lakini tutafanya marekebisho ya kimuundo pamoja kupendekeza vyanzo vya mapato,” alieleza bwana Mfugale na kuongeza:
“Sheria hii iliyopo inasema kila halmashauri inatakiwa kutoa mchango wa asilimia 10 kwa awamu moja tu, yaani wakishatoa hiyo asilimia ni basi, hivyo kuna kila sababu ya kuona namna nyingine ya kurekebisha hili.”
Aliongeza kuwa wao kama Bodi wamependekeza sheria mpya kuzitaka kila halmashauri kutoa mchango wa asilimia moja ya mapato yake ya ndani kila mwaka na iwapo itachelewesha mchango huo itatakiwa kulipa na riba ya ziada.
“Lakini pia Sheria ya sasa inamtaka mkopaji kulipa asilimia 13 tu ya riba kitu ambacho siyo sawa kuweka kiwango cha riba katika sheria kwa kuwa sio mara zote fedha za mkopo zinatoka katika bodi, kwani mara nyingine hata sisi tunakopa,” alisema Mfugale na kuongeza:
“Riba itategemeana na gharama za mkopo huo, kwa hiyo ni afadhali sheria iseme kuwa riba itakuwa ya gharama nafuu kuliko kutaja kiwango kama ilivyo sasa.”
Mfugale alisema kuwa Bodi imeonelea kuifanyia marekebisho sheria hiyo kwani imepitwa na wakati na hivyo kuisababishia Bodi hiyo changamoto ya ufinyu wa fedha hali inayopelekea kushindwa kufanyia kazi maombi yote ya mkopo wanayopokea kutoka katika halmashauri mbalimbali nchini.
Katibu wa bodi hiyo alivitaja vyanzo vya mapato vya bodi hiyo kuwa ni michango ya halmashauri kupitia mapato yao ya ndani, riba inayotokana na mikopo kwa halmashauri pamoja na ruzuku kutoka serikali kuu lakini fedha hizo ni kidogo ikilinganishwa na mahitaji ya bodi yaliyopo.
Alisema kufikia sasa Bodi yake imekwishapokea maombi ya mkopo wa shilingi Bilioni 50 kutoka halmashauri kadhaa lakini imeweza kutoa mkopo wa shilingi Bilioni 5.7 tu hali inayokwamisha malengo waliojiwekea.
“Mbali ya hiyo Bilioni tano tuliyoitoa lakini kuna shilingi Bilioni tano tunatakiwa kupata kama michango kutoka mamlaka za serikali za Mitaa, kwa ujumla wake bado haiwezi kukidhi mahitaji yetu ya Bilioni 50 zilizoombwa miaka kadhaa iliyopita” alisema Mfugale.
Alisema kwa kiwango kikubwa changamoto hiyo inachangiwa na sheria inayotumika kwa sasa kwani imepitwa na wakati na hivyo inahitaji marekebisho ili kukidhi mahitaji ya sasa.
Mbali na changamoto hizo za kisheria Mfugale alisema pia wanakumbana na changamoto nyingine ya marejesho ya mikopo kutoka kwa halmashauri kwani nyingi ulipaji wake ni wa kusuasua.
“Halmashauri zinazolipa vizuri hazizidi 60, zaidi ya mia zinasumbua, na hii inatokana na vipaumbele, hawajaweka kipaumbele katika suala hilo la malipo wakati suala hili lipo kisheria na sio suala la kusubiri kikao chochote”
Kufuatia hali hiyo Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Selemani Jafo alizipiga mafuruku halmashauri zinazodaiwa na Bodi kuacha kukopa katika taasisi nyingine za fedha hadi hapo watakapomaliza kulipa madeni wanayodaiwa na Bodi ya Mikopo ya Serikali za Mitaa ambapo halmashauri zinazodaiwa zimeonyesha kutii agizo hilo.
Haki Miliki@ Bodi ya Mikoya Mikopo ya Serikali za Mitaa