Waziri Jafo Aitaka Mikoa Kusimamia Lishe Ili Kupunguza Udumavu
Nteghenjwa Hosseah, OR-TAMISEMI.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR TAMISEMI), Mhe. Selemani Jafo (Mb) amewaongoza wakuu wa Mikoa yote Tanzania Bara, kupitia na kusaini Mkataba wa Utendaji kazi na Usimamizi wa shughuli za Lishe kwa kila mkoa katika kikao kazi kilichofanyika mjini Dodoma na kuwaomba wakasimamie suala la Lishe kwa nguvu zote.
Akiongea na Wakuu wa Mikoa katika ofisi za Wizara hiyo mjini Dodoma, Mhe. Jafo amesema maelekezo hayo awali, yalitolewa na Mhe. Makamu wa Rais wa Tanzania Mama Samia Suluhu, kuhusu tatizo la Lishe katika Mikoa na Kwa sasa Taifa limeamua kulishughulikia na Fedha imetengwa katika bajeti ya mwaka wa fedha 2017/2018.
“Tumesaini hii mikataba kwa lengo kubwa la kuhakikisha kwamba Wakuu wa Mikoa kama viongozi wa Wakuu wa Mikoa, wahakikishe halmashauri zao zinaenda kutekeleza mipango yao ya bajeti ambayo imetengwa katika halmashauri zao hususan ni suala la Lishe ambalo kwa sasa ni agenda kubwa na tutataka tuisimamie ili kuondoa Udumavu katika jamii zetu.
Mhe. Jafo amesema Wakuu wa Mikoa wanayo dhamana kubwa ya kusimamia miradi ya maendeleo kama ujenzi wa vituo vya afya na suala la lishe kwa ujumla, hivyo Watendaji watoe taarifa zao kwa Wakuu wa Wilaya kabla ya kuwasilishwa kwa Wakuu wa Mikoa kwa hatua stahiki.
“Wakurugenzi watoe taarifa kwa Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Wilaya nao wawasilishe kwa Wakuu wa Mikoa ili waone namna ya kuzisemea taarifa hizo katika suala zima la utekelezaji wa mipango ya Serikali”.
Aidha, amewataka Wakuu wa Mikoa kuwaelekeza na kuwasimamia Wakurugenzi wa Halmashauri kwa ajili ya masuala ya lishe na ujenzi wa vituo vya afya 2011 ambavyo mpaka sasa vimeboreshwa na kujengwa ili kutoa huduma bora kwa jamii.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dkt. Kebwe S. Kebwe amesema, anaipongeza Serikali kwa kutoa takribani shilingi 11.6 Bilioni kwa ajili ya suala la lishe hasa katika kipengele cha udumavu.
Aidha, amesema suala zima la upatikanaji wa chakula mkoani Morogoro sio tatizo bali ni elimu ya ulaji chakula ndiyo inapaswa kutolewa ili kupunguza utapiamlo lakini pia kumekuwepo na tatizo la Maafisa Lishe katika halmashauri nchini kupangiwa kazi nyingine, kwa mfano kufanya kazi ya Idara tofauti kama vile kukusanya kodi.
Naye Stephen Motambi, Kaimu Mkurugenzi anayeshughulikia masuala ya Lishe Ofisi ya Rais TAMISEMI, amesema suala la Lishe limekuwa likifanyika katika Mikoa na Halmashauri zote katika kukabiliana na tatizo hili lakini kwa hivi sasa hali ya udumavu ni asilimia 34 hivyo mikoa inapaswa kuweka mikakati kuhusiana na kuondoa kabisa tatizo la lishe.
Haki Miliki@ Bodi ya Mikoya Mikopo ya Serikali za Mitaa